Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba ahadi alizotoa kwa Wananchi wa Jimbo hilo wakati akiwatumikia ndani ya Kipindi cha Miaka 10 iliyopita atahakikisha kwamba anazikamilisha kabla ya kuanza kwa  kipindi chengine cha Uongozi  baada ya kumalizika kwa uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba mwaka huu.

Alisema yeye bado anaendelea kuwa Kiongozi wa Jimbo hilo kwa vile jukumu la kuwatumikia Wananchi wa Maeneo hayo  uko mikononi mwake na wala hafanyi kampeni kwa mujibu wa kanuni kwa vile muda wa kufanya hivyo haujafika licha ya kwamba unakaribia.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Kiomba Mvua katika hafla fupi ya kukabidhi mchango wa shilingi Milioni 5,000,000/- kwa Uongozi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } zitakazotumika katika ujenzi wa Kibanda kwenye Kisima Kilichochimbwa na Mamlaka hiyo kitakachosambaza maji katika kijiji hicho na vile vya jirani.

Alisema Wananchi wa Kijiji cha Kiomba Mvua wamekuwa wakikabilia na tatizo la huduma za maji safi na salama kwa kipindi kirefu ambapo yeye kama kiongozi aliwaahidi kufanya juhudi kwa kushirikiana  na washirika wa maendeleo kutatua changamoto hiyo ya muda mrefu.

Akipokea mchango huo wa shilingi Milioni 5,000,000/- Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar Dr. Mustafa Garu alisema Mamlaka hiyo inaendeleza jitihada za kuimarisha miundo mbinu ya sekta ya Maji ili kuwaondoshea usumbufu unaowapata Wananchi katika baadhi ya maeneo hapa Nchini.

Wakati huo huo Balozi Seif Ali Iddi alikabidhi mchango wa Shilingi Milioni 5,000,000/-  akitekeleza ahadi aliyotoa ya kusaidia kuifanyia matengenezo makubwa Ofisi ya Tawi la Chama cha Mapinduzi ya Kinduni.

Akizungumza katika hafla hiyo fupi  Balozi Seif  aliwakumbusha  Viongozi pamoja na Wanachama wa CCM wa Tawi hilo kuwachagua Viongozi makini watakaokubali kushirikiana na Wananchi katika harakati za maendeleo yao.

Akipokea mchango huo kwa Niaba ya Wanachama hao wa Chama cha Mapinduzi Tawi la Kinduni Katibu wa CCM wa Tawi hilo Nd. Shaaban Mohammed alimpongeza Balozi Seif kwa uungwana wake wa kutekeleza ahadi anazotoa katika kipindi kifupi.

Mapema Mke wa Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope Mama Asha Suleiman Iddi  alisema jukumu la kuwachagua Viongozi  bora wanaofaa kusimamia changamoto zinazowakabili  Wananchi limo mikononi mwa Akina Mama.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...