Na. Richard Bagolele- Chato

Baadhi ya wananchi wilayani Chato wameipongeza serikali kupitia mpango wa TASAF Awamu ya tatu wa kunusuru kaya masikini. Wakiongea kwa nyakati Tofauti wananchi hao kutoka kata ya Bwongera ambao ni wanufaika wa Mpango huo wamesema Mpango wa TASAF Awamu ya tatu ni mkombozi kwa wananchi masikini na wameahidi kutumia pesa hizo kwa manufaa ya familia na mahitaji muhimu ya huduma za afya na elimu kwa watoto wao.

“Tunaishukukuru serikali yetu kwa huu mpango mzuri ambao matunda yake tunayaona hapa hapa, nimepokea hela mwezi uliopita nimenunua mbuzi watatu, malipo ya awamu hii nitaboresha nyumba yangu” alisema Bibi Tabu Paulo mkazi wa kijiji cha Mkolani kata ya Bwongera.

Kwa upande mwingine baadhi ya wanufaika wa mpango huo wamelaumu baadhi ya akina baba ambao wamekuwa wakiwalazimisha wenzi wao kutokwenda kuchukua fedha hizo na badala yake wakina baba ndiyo wamekuwa wakitaka kukabidhiwa fedha hizo ambapo ni kinyume na mwongonzo wa mpango wa TASAF awamu ya tatu ambao unawataka wakina mama kama wawakilishi wa kaya wapokee fedha hizo kwa niaba ya familia.

Mratibu wa TASAF wilayani Chato Bw. Alex Manga’ra amesema tangu kuanza kwa zoezi la ulipaji fedha kupitia mpango huo wamekutana na changamoto hiyo ambapo amesema utaratibu wa nani anapaswa kupokea fedha hizo tayari ulikwishaelezwa kwenye mikutano ya serikali za vijiji na mikutano mikuu ya vijiji vyote vinavyonufaika na mpango huo lakini akina baba wamekuwa wakitaka kulipwa wao badala ya akina mama. Hata hivyo Bw. Manga’ra ameahidi kuendelea kutoa elimu kwa wanufaika wa mpango ili tatizo hilo lisiendelee kujirudia.

Naye Msimamizi Mshauri wa Mpango kutoka TASAF Bw. Richard Komba ameziomba kaya zinazonufaika na mpango kutokufumbia macho pindi waume zao wanapowakataza kwenda kupokea fedha hizo na kuwataka wawasiliane na wawakilishi wa serikali ya kijiji ambao wamo kwenye mpango ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.

Mpango wa TASAF Awamu ya tatu ulizinduliwa mwezi January 2014 na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Rodrick Mpongolo na mchakato wa kubaini kaya masikini ulianza mapema mwaka huu ambapo kaya Zaidi ya 8000 kutoka vijiji 71 wilayani hapa ziliibuliwa na kuthibitishwa kupitia mikutano mikuu ya vijiji na Hatimaye kukidhi vigezo vya kaya masikini.
Bibi Tabu Paulo mkazi wa kijiji cha Mkolani kata ya Bwongera ambaye baada ya kupokea fedha za awamu ya kwanza kupitia mpango wa TASAF III alinunua mbuzi 3 kama njia ya kujikwamua na umasikini.
Bibi Sesilia Bernado (kulia) mkazi wa kijiji cha Mkolani kata ya Bwongera ambaye baada ya kupokea fedha za awamu ya kwanza kupitia mpango wa TASAF III alinunua mabati 6 ili aboreshe makazi yake.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...