Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa,akisisitiza jambo kwa Menejimenti ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), alipokutana nao kabla ya kuongea na Wafanyakazi.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (mwenye koti la kaki), akisisitiza jambo kwa Wafanyakazi wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL),alipokutana nao jijini Dar es Salaam.
 Rubani Lilla Borri wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), akisisitiza jambo wakati wa mkutano wa Wafanyakazi wa Shirika hilo na Waziri Prof. Mbarawa, uliofanyika  katika ofisi za Shirika hilo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akiagana na Wafanyakazi wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), mara baada ya kuongea nao Ofisini Hapo.

SERIKALI imezungumzia umuhimu wa kulifufua upya Shirika la Ndege nchini Air Tanzania (ATC) kwa kulinunulia ndege mpya na kulipa mtaji ili lifanye kazi kibiashara na kutengeneza faida kama ilivyokusudiwa awali.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (Pichani)ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na menejimenti na wafanyakazi wa Shirika hilo alipolitembelea jijini Dar es Salaam leo.

“Tutawekeza kwenye Air Tanzania ili kuongeza fursa za kiuchumi na kuvutia wasafiri wengi kufika nchini moja kwa moja na kuvutia sekta ya utalii”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Waziri Prof. Mbarawa amewataka wafanyakazi wa Shirika hilo ambao sio waadilifu na wavivu kuondoka mara moja ili kupisha wafanyakazi wabunifu na wenye mawazo ya kibiashara kuendesha shirika hilo kwa faida.

“Tunataka watu watakaolitoa shirika hili kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa kuliwezesha kiuchumi na kujitegemea ili kushindana na mashirika mengine ya ndege katika biashara“, amesisitiza Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Magufuli yuko tayari kununua ndege mpya ili kulifufua shirika hili hivyo amewataka wafanyakazi hao kuwa na mtazamo chanya wa kufanya biashara ili kuiletea taifa tija.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa ATC Bw. Johnson Mfinanga amemwambia Waziri Prof. Mbarawa kuwa kwa sasa shirika hilo lipo katika hali mbaya kiuchumi na hivyo kuhitaji nguvu ya Serikali kulikwamua ili litoe huduma inayoshahili.

Aidha, Waziri Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa Serikali itaangalia upya taratibu za ajira katika shirika hilo na watakaobainika kuajiriwa kinyume cha taratibu watafukuzwa kazi mara moja.

“Tutanataka watu waadilifu, wabunifu na wenye sifa stahiki ili wafanye kazi kwa maslahi ya shirika na taifa kwa ujumla”, amefafanua Waziri Mbarawa.

Shirika la Ndege nchini ATC toka mwaka 2009 limekuwa likijiendesha kwa hasara na Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kulifufua shirika hilo ili lifanye kazi kwa faida na kuboresha usafiri wa anga ndani na nje ya nchi na hivyo kuvutia wasafiri wengi kuja nchini moja kwa moja.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Pongezi kwako Rais wetu Magufuli na serikali kwa ujumla pigeni kazi kwa uzalendo nyie wafanyakazi na muwe mnajisikia#aibu kwanini watu wa Adis Ababa au #Kigali waweze sisi tushindwe? so jiulizeni hayo maswali kisha mtapata ujasiri na #uzalendo na mabadiliko tutayaona soon as possible mimi naitwa the Mdudu niko huku UGAIBUNI England ukipenda ita uingereza kilio changu ndugu zangu mimi nataka kujivunia changu so nataka kuya paramia ma Air Tanzania from London to Dar na wala sivinginevyo

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...