Kamati ya Rufaa ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), leo Mei 3, 2016 imetupilia mbali rufaa saba kati ya nane zilizowasilishwa mbele yake na viongozi, mchezaji na timu tatu zilizoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara 2015/2016 maarufu kama StarTimes League.
Kaimu Mwenyekiti wa kamati, Wakili Revocatus Kuuli ametangaza uamuzi mbele ya waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Mikutano wa ofisi za TFF, zilizoko kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam. 
Uamuzi huo unatokana na kikao cha akidi iliyotimia ya Kaimu Mwenyekiti wa Kamati, Wakili Revocatus Kuuli pamoja na wajumbe wawili, Dk. Francis Michael na Abdallah Shaweji. Kadhalika warufani wote walihudhuria kikao hicho kilichojadili rufaa hizo Jumapili Mei mosi, 2016.
Kamati imemtoa hatiani Kipa wa Geita Gold, Denis Richard Dioniz baada ya kujiridhisha kuwa haikuwa jukumu lake kupanga muda wa mchezo kwa mujibu wa kanuni kutokana na kutumia muda mrefu maliwato baada ya kuugua tumbo kama ilivyoripotiwa na mwamuzi na kamisaa wa mchezo.
Dioniz alifungiwa miaka 10 kutojihusisha na mpira wa miguu sambamba na kulipa faini ya shilingi milioni kumi (10,000,000). Adhabu hiyo alipewa na pamoja na Kipa Mohamed Mohamed wa JKT Kanembwa. Mohamed hakukata rufaa baada ya kuadhibiwa Aprili 3, 2016.
Wadau hao wa soka walikata rufaa dhidi ya uamuzi wa Kamati ya Nidhamu baada ya kamati hiyo kuwatia hatiani na kuwaadhibu kwa makosa ya kupanga matokeo ya michuano ya Ligi Daraja la Kwanza. Ambao rufaa zao zimetupwa ni:
Timu ya Geita Gold
Choki Abeid ambaye ni Kocha Msaidizi wa timu ya soka ya Geita Gold FC
Fatel Rhemtullah – Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tabora
Saleh Mang’ola – Mwamuzi wa Soka wa Mkoa wa Dodoma
Timu ya Soka ya Polisi Tabora
JKT Oljoro Fc ya Arusha
Yusufu Kitumbo – Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Tabora
Katika adhabu hizo leo Kamati ya Rufaa ya Nidhamu imebariki adhabu kwa Choki Abeid ambaye ni Kocha Msaidizi wa timu ya soka ya Geita Gold FC aliyetiwa hatiani kwa kumshawishi Mohammed - kipa wa JKT Kanembwa FC kukaa golini ili penalti aliyogomea kabla ipigwe.
Awali, Kamati ya Nidhamu imewafungia maisha kutojihusisha na mpira wa miguu mwamuzi wa mchezo kati ya JKT Kanembwa FC v Geita Gold, Saleh Mang’ola Saleh Mang’ola – Mwamuzi wa Soka wa Mkoa wa Dodoma
Kuhusu Yusufu Kitumbo – Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Tabora na Fatel Rhemtullah ambaye ni Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tabora hao imeamuriwa kuendelea kutumikia adhabu ya kufungiwa maisha kutojihusisha na mpira wa miguu kama Mwenyeakiti wa klabu ya JKT Oljoro, Amos Mwita na kocha msaidizi wa Polisi Tabora, Bernad Fabian
Klabu za Geita Gold (Geita), JKT Oljoro (Arusha) na Polisi Tabora (Tabora) zilikutwa na hatia ya upangaji wa matokeo na kupewa adhabu ya kushushwa daraja mpaka ligi daraja la pili (SDL) msimu ujao, hivyo kamati imeamuru adhabu hiyo iendelee.
Uamuzi wa Kamati ya Nidhamu ya TFF Aprili 3, 2016 ilitoa uamuzi wa shauri la upangaji wa matokeo wa kundi C kwa Ligi Daraja la Kwanza. Aliyesoma hukumu hiyo ni Wakili Jerome Msemwa ambako alisema adhabu hizo zimetolewa kwa kufuata Kanuni za Nidhamu za TFF, na nafasi ya kukata rufaa kwa wahusika juu ya maaamuzi hayo ziko wazi.
Upande wa klabu ya JKT Kanembwa FC ya mkoani Kigoma, imeshushwa daraja mpaka kwenye ngazi ya ligi ya mkoa (RCL), baada ya kushika nafasi ya mwisho katika msimamo wa kundi lake, Kundi C sambamba na kumfungia maisha kutojihusisha na mpira wa miguu kamisaa wa mchezo wa Geita Gold na JKT Kanembwe, Moshi Juma baada ya kukutwa na hatia ya upagaji matokeo.
Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Geita (GEREFA), Salum Kurunge, Mwenyekiti wa klabu ya Geita Gold, Cosntantine Moladi na Katibu wa klabu ya JKT Kanembwa Basil Matei waliachiwa huru na Kamati ya Nidhamu baada ya kutokutwa na hatia katika shauri hilo.
Mwamuzi wa mchezo kati ya Polisi Tabora v JKT Oljoro, Masoud Mkelemi na mwamuzi wa akiba, Fedian Machunde walifungiwa kwa muda wa miaka kumi kutojihusisha na mpira wa miguu, na kutozwa faini ya shilingi milioni (10,000,000) kumi kila mmoja.
Katibu wa klabu ya Polisi Tabora, Alex Kataya, Katibu wa klabu ya JKT Oljoro, Hussein Nalinja, mtunza vifaa wa klabu ya Polisi Tabora, Boniface Komba, na Meneja wa timu ya  Polisi Tabora, Mrisho Seleman, waliachiwa huru na Kamati ya Nidhamu ya baada ya kutokutwa na hatia. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...