Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete leo ametoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha Waseda kilichoko jijini tokyo, Japan kufuatia mwaliko wa Taasisi ya Association of African Economy and Development (AFRECO) ya Japan. Muhadhara huo ulihusu Uhusiano kati ya Japan na Afrika kuelekea kilele cha mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo Africa (TICAD) utakaofanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika tarehe 27-28 Agosti jijini Nairobi.

Akizungumza na wanafunzi, wanataaluma na mabalozi wa nchi za Afrika walioko Japan, Rais Mstaafu Kikwete ameelezea hali ya uhusiano mzuri ulioko baina ya Japan na Afrika. 

Ameipongeza Japan kwa kuwa moja ya nchi chache ambazo hazikuondoa matumaini yake kwa bara la Afrika wakati ambapo Afrika ilipita katika kipindi kigumu cha kupoteza umuhimu wake machoni mwa mataifa makubwa, baada ya kwisha kwa vita baridi ya dunia mwanzoni mwa miaka ya 1990. Ni katika kipindi hicho, mnamo mwaka 1993 ambapo Japan ilianzisha mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika. Utaratibu huo umekuja kuigwa na mataifa mengine duniani.
Rais Mstaafu Dk. Jakaya Mrisho Kikwete akiwasili Wasuda University Kutoka kushoto ni Seneta Mstaafu Tetsuro Yano, Balozi Mathias Chikawe, Bi.Kyoko Hasegawa na Afisa Ubalozi Francis Mossongo.

Akielezea hali ya maendeleo barani Afrika, Rais Mstaafu ameelezea kutiwa moyo na mafanikio ambayo bara la Afrika imeyapata katika kipindi cha miaka 15 ambako pato la taifa limekuwa mara dufu kutoka wastani wa asilimia 2 katika miaka ya 1980 hadi 1990 hadi kufikia asilimia 5 kati ya mwaka 2001 na 2014. 

Hata hivyo amekumbusha kuwa, kutokana na bara la Afrika kuwa nyuma sana kwa kipindi kirefu, bado safari ya Afrika kujitegemea ni ndefu mno na hapana budi bara la Afrika kusaidiwa kufupisha urefu wa safari hiyo. Kwa hilo, ameipongeza Japan kwa kuongeza mara dufu misaada yake kwa bar ala Afrika kutoka kiasi cha dola za kimarekani milioni 900 mwaka 2007 hadi dola za kimarekani bilioni 1.8 mwaka 2011, huku Mitaji ya Uwekezaji ikiongezeka pia mara dufu kutoka dola za kimarekani bilioni 3.4 hadi dola za kimarekani bilioni 6.2 mwaka 2011 kama ilivyoahidiwa katika Mkutano wa IV wa TICAD.
Rais Mstaafu Dk. Jakaya Mrisho Kikwete akitoa muhadhara katika Chuo Kikuu cha Waseda jijini Tokyo mapema leo.

Pamoja na kupongeza jitihada hizo, Rais Mstaafu Kikwete amehimiza juu ya umuhimu wa Japan kuwekeza zaidi barani Afrika hususan kushajihisha Sekta Binafsi ya Japan kufanya hivyo. Amesema, pamoja kuongezeka kwa uwekezaji wa Japan barani Afrika kutoka dola za kimarekani milioni 758 mwaka 2000 hadi dola za kimarekani bilioni 10 mwaka 2014, kiwango hicho kilichowekezwa katika bara la Afrika lenye nchi 54 bado ni kidogo ikilinganishwa na kiasi cha dola za kimarekani bilioni 20 ambacho Japan imewekeza katika nchi 6 tu za Singapore, Thailand, Malaysia, India, Philipines na Vietnam katika kipindi cha miaka 5 iliyopita.

Ameshauri Mkutano wa Sita wa TICAD utakaofanyika Nairobi pamoja na mambo mengine ujikite katika kuchochea uwekezaji wa Japan barani Afrika kwa kujengea uwezo nchi za kiafrika kufany abiashar ana Japan, kuona uwezekano wa kuanzisha Mfuko Maalum wa Kusaidia Uwekezaji wa Sekta Binafsi ya Japan barani Afrika, kurahisisha muingiliano wa kibiashara baina ya wafanyabiashara wa Japan na Afrika, na kuwekeza katika vijana wa pande zote mbili na kuwaunganisha ili kuendeleza mashirikiano yaliyokuwepo baina ya pande mbili.
Rais Mstaafu Dk. Jakaya Mirsho Kikwete akimsikiliza mwanafunzi katika kipindi cha maswali na majibu.

Rais Mstaafu amemalizia kwa kusihukuru Serikali ya Japan na watu wake kwa kuunga mkono jitihada za Tanzania katika kujiletea maendeleo. Amewashukuru wajapani kwa kusaidia ujenzi wa miundombinu ya barabara, ujenzi wa barabara ya juu ya TAZARA (FlyOver), ujenzi wa miradi ya umeme ya Kinyerezi II, Miundo mbinu ya kuunganisha Umeme ya kati ya Kenya na Tanzania na miradi mingine ya maendeleo. 

Amewashukuru kwa misaada inayotolewa na Serikali ya Japan nchini Tanzania inayofikia Yeni bilioni 41.9.Amehitimisha kwa kusema kuwa hatma ya uhusiano baina ya Japan na Afrika iko mikononi mwa vijana wa pande zote mbili.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...